Emmaus Shule ya Biblia kwa Njia ya Posta

Emmaus Shule ya BibliaEmmaus Shule ya Biblia kwa Njia ya Posta inahudumia watu wote wanaopenda kusoma Biblia kwa njia ya posta. Masomo na mitihani yanatumwa kwa mwanafunzi. Baada ya kujaza anarudisha mtihani kwenye ofisi zetu.

Ilianzishwa kwa mara ya kwanza Tanzania mwaka 1960. Inafundisha Biblia kwa watu wa aina zote, na waumini wa dini zote. Haifundishi misingi wala mitazamo ya dhehebu lolote, bali ujumbe wa Neno la Mungu jinsi lilivyo.

Jina EMMAUS linatokana na jina la kijiji kimoja katika Biblia ambako wanafunzi wawili walikuwa wanaelekea walipotokewa na Bwana Yesu alipofufuka, Luka 24:13.

Kijiji hicho kiliitwa Emau kwa Kiswahili, na Emmaus kwa Kiingereza. („Emmaus“ ni tofauti kabisa na shirika la EMAU Tanzania ambalo ni kifupisho cha „Elimu ya Malezi ya Ujana“. Ili kuondoa utata, shule hii inatumia jina la Kiingereza, EMMAUS.)

 

Lengo la EMMAUS ni nini?

Wanafunzi wawili waliosafiri kwenda Emau (Emmaus), Bwana Yesu alipowatokea aliwafundisha mambo yaliyomhusu YEYE MWENYEWE; Luka 24:27. Hilo ndilo lengo kubwa la shule ya Emmaus: Kuwafundisha mambo yanayomhusu Mwokozi, na kuwaelekeza jinsi ya kukutana naye ili waweze kusema pia, „Je! mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?“ (Luka 24:32).

 

Mwanafunzi wa EMMAUS

Emmaus Emmaus Shule ya Biblia DodomaNi mtu gani anayeweza kujiunga kuwa mwanafunzi wa EMMAUS? Mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika anakaribishwa kujifunza masomo ya EMMAUS.

Sasa hivi EMMAUS ina wanafunzi 2,000 walio katika marika mbalimbali, kuanzia wanafunzi wa Shule za msingi mpaka watu wazima waliostaafu kazi. Wengine ni wakulima, wengine wafanya kazi wa nyumbani, wafanya biashara, waajiriwa maofisini, walimu, askari, n.k.